Wakizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Waislamu wa Masjid Ahlul-Bayt (as) Nshambya, Ndugu Twahiri Ghataya na Viongozi wengine wa Masjid hii wametumia fursa hii kuwatakia watu wote heri, baraka, na mafanikio mema katika maisha yao, huku wakikumbusha maadili ya kusameheana, kusaidiana na kuendeleza mshikamano wa kijamii.
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Baut (as) -ABNA- Bukoba Mjini, 7 Juni 2025 – Waislamu wa Masjid Ahlul-Bayt (as) Nshambya, Bukoba Mjini, wametuma salamu za Eid Mubarak kwa jamii zote za Kiiislamu hapa nchini Tanzania na duniani kote kwa ujumla katika kuadhimisha sikukuu ya Eid Al-Adh’ha. Katika ujumbe wao wa sikukuu, Waumini wa Masjid haya wamesisitiza umuhimu wa kusherehekea Eid hii kwa moyo wa mshikamano, amani, na upendo wa Kiislamu.
Wakizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Waislamu wa Masjid Ahlul-Bayt (as) Nshambya, Ndugu Twahiri Ghataya na Viongozi wengine wa Masjid hii wametumia fursa hii kuwatakia watu wote heri, baraka, na mafanikio mema katika maisha yao, huku wakikumbusha maadili ya kusameheana, kusaidiana na kuendeleza mshikamano wa kijamii.
Eid Al-Adh’ha ni tukio la kiroho lenye umuhimu mkubwa katika maisha ya Waislamu, likiwa ni kumbukumbu ya imani, kujitolea, na kujisalimisha kwa amri za Mwenyezi Mungu kama alivyofanya Nabii Ibrahim (as). Waumini wa Masjid Ahlul-Bayt (as) Nshambya wametilia mkazo umuhimu wa kuwasaidia maskini na wahitaji katika kipindi hiki, ili kila mtu aweze kusherehekea na kufurahia furaha ya Eid.
Katika ujumbe wao, wametoa wito wa kudumisha hali ya utulivu na amani katika familia, jamii, na taifa kwa ujumla wakati wa sikukuu hii, pamoja na kuenzi maadili mema yanayohimiza upendo, heshima na mshikamano miongoni mwa watu wote bila ubaguzi.
Masjid Ahlul-Bayt (as) Nshambya inaendelea kuwa nguzo muhimu ya kiroho na kijamii katika Mji wa Bukoba, ikiwahamasisha waumini wake na jamii kwa ujumla kushiriki katika shughuli za maendeleo, elimu, na ibada, hasa katika nyakati za sikukuu hizi muhimu za Kiislamu.
Kwa ujumla, salamu za Eid Mubarak kutoka Masjid Ahlul-Bayt (as) Nshambya zinahimiza watu wote kuenzi sikukuu hii kwa moyo wa amani, shukrani, na kutoa sadaka kwa wenye uhitaji, ili baraka za Eid ziweze kuenea kwa wote.
Your Comment